Kuhusu MALAS
Kuhusu MALAS COMMUNITY
MALAS ni asasi na jumuiya inayojumuisha vijana katika sekta ya utalii ambayo lengo ni kutangaza utalii na vivutio vya utalii, kufanya shughuli za utalii, utamaduni, uhifadhi mazingira, na kijamii. Pia, MALAS COMMUNITY tunafanya kunadi maeneo mbalimbali kwenye masoko ya kijamii, kitalii, kiuchumi, na mengineyo.
Historia kwa ufupi
MALAS ADVENTURES COMMUNITY ilianzishwa mwaka 2018 kama programu tu iliyokuwa inatoa elimu ya athari za ujangili wa wanyamapori hasa tembo na faru. Ilijikita mtandaoni pekee (Facebook pekee). Mwanzilishi ni James Manventure.
Mwaka 2021 ndipo ilianzishwa rasmi na kuanza kupata wanachama, wakati huo inaitwa WILDLIFE AMBASSADOR. Mwaka 2024 jina lilisajiliwa BRELA (Namba ya usajili. 563837) na baadae ikabadilishwa rasmi na kuitwa MALAS ADVENTURES COMMUNITY.
- Imeanza mwaka 2021 kama program kwenye Facebook
- MALAS imesajiliwa BRELA mwaka 2024
- Hadi sasa tunafanya ziara na kuandika makala za uhifadhi


Ikiwa bado ni program kwenye mitandao ya kijamii ilikuwa chini ya mtu mmoja pekee. Mwishoni mwa mwaka 2021 ikawa timu ya watu wawili, ndipo mwaka 2022 hadi mwaka 2023 timu ikaongezeka hadi kufika watu sita kutokea mikoa tofauti, yaani Dar es Salaam, Songea, Dodoma, na Morogoro.
Mwaka 2024 ukawekwa mkakati wa kutoka kuandika tu makala mitandaoni na kuanza kufanya kazi katika hali ya kawaida, yaani kukutanisha vijana na wanafunzi wenye mapenzi na utalii pamoja. Kuanzia hapo hadi sasa JUMUIYA YA MALAS (MAC) tunakutanisha vijana wenye ujuzi wa kuandika makala mbalimbali za utalii, mazingira, utamaduni, na wanyamapori.
USHIRIKI KWENYE SHUGHULI MBALIMBALI
1. Ushiriki katika tuzo (Awards)
Jina la MALAS COMMUNITY likiwa bado ni program inaitwa WILDLIFE AMBASSADOR tumepata nafasi kadhaa za kushiriki kwenye tuzo mbalimbali Tanzania.
Mwezi Mei 2022 tumeshiriki katika UDOM AWARDS 2022 kwenye kipengele cha "BEST SOCIAL MEDIA PAGE". Mwezi Agosti 2022 katika tuzo za Tanzania Emerging Youth Awards (TEYA 2022), Dar es Salaam. Ndugu Manventure alishiriki tuzo kwa kutumia brand ya WILDLIFE AMBASSADOR kwenye kipengele cha "YOUTH CHAMPION IN TOURISM" na kushika nafasi ya nne.
Mwaka 2024 ndugu Manventure alishiriki tuzo za YOUTH IN BUSINESS AWARDS, jijini Dodoma kwenye kipengele cha "MOST YOUTH IN TOURISM" na kushika nafasi ya pili. Kwenye tuzo hizo zote hatukunyanyua kombe lakini tumekutanishwa na watu ambao wamekuwa chachu ya sisi kupiga hatua kubwa kwenye utalii.
2. Kampeni za Utalii
Mwezi Aprili mwaka 2025 vijana wa MALAS ADVENTURES COMMUNITY walishirikiana na TANAPA mkoa wa Dodoma kuzungukia maeneo mbalimbali ya Dodoma kwenye kampeni ya VOTE NOW. Kampeni hii huandaliwa na TANAPA kwa lengo la kuhamasisha wanachi kupigia kura vivutio vya utalii vinavyowania ushindi katika tuzo za WORLD TRAVEL AWARDS.
Kwa kushirikiana na TANAPA mkoa wa Dodoma tumeweza kuwafikia wanafunzi wa vyuo vifuatavyo; The University of Dodoma (UDOM), Institute of Rural Development Planning (IRDP - MIPANGO), College of Business Education (CBE - Dodoma campus), na St. John's University of Tanzania (Dodoma campus). Tunashukuru Uongozi wa TANAPA mkoa wa Dodoma kutuamini na kutushirikisha katika kampeni hii. Mengi zaidi yatazidi kufanyika.
Imekuwa ni nafasi adhimu na ya upekee sana kwetu Jumuiya ya MALAS kwa sababu inadhihirisha ukomavu wa safari tuloianza ya kutangaza na kunadi vivutio vya utalii Tanzania. Malengo na matamanio yetu ni kushirikiana na taasisi nyingi zaidi zinazohusika na uhifadhi pamoja na utalii ndani ya Tanzania na hata nje ya mipaka ya Tanzania.
3. Safari za kitalii na kujifunza
Siku ya jumamosi, tarehe 12 Aprili, 2025 tulifanikisha kuandaa safari ya wanafunzi kutoka UDOM kwenda kutembelea Ofisi ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kanda ya kati zilizopo Dodoma mjini. Jumla ya wanafunzi themanini waliweza kuhudhuria safari hii iliyokuwa na lengo la kujifunza majukumu ya Bodi ya Utalii Tanzania na kujifunza Utalii wa Tanzania.
MALAS Community tukiwa ofisi za TTB tumejifunza mambo mengi na fursa zilizopo kwenye sekta pendwa ya utalii. Safari hii moja imefungua milango kwa kupanga safari nyingine nyingi zaidi zitakazo ratibiwa na kuandaliwa nasi.
Mwaka 2024 hadi sasa
Kuanzia tarehe 1 Disemba 2024 rasmi jina la MALAS ADVENTURES COMMUNITY lilianza kutumika badala ya jina WILDLIFE AMBASSADOR. Timu ilianza mchakato wa kubadili jina kutokana na sababu kadhaa ambazo zilipelekea jina WILDLIFE AMBASSADOR kuwa na mipaka kwenye utekelezaji wa program za utalii. sababu kuu ikiwa ni jina lenyewe linasadifu wanyamapori, yaani "Balozi wa Wanyamapori". Na timu ilifikia uhitaji wa kutangaza vivutio vya utalii kwa ujumla.
Ili kuwa na nafasi nzuri katika kutangaza utalii na utamaduni, jina likabadilishwa na kuwa MALAS ADVENTURES COMMUNITY. Januari 2025 tukabadili na kuhuisha taarifa za usajili BRELA. Rasmi sasa tunaitwa JUMUIYA YA MALAS (MALAS COMMUNITY) - Jumuiya inayofanya kazi kwa hiari kunadi na kutangaza vivutio vya utalii. Pia uandishi wa makala za utalii na utamaduni kwa lugha mbalimbali, lakini lugha kuu ikiwa ni Kiswahili.

JUMUIYA YA MALAS kufikia vijana na vikundi vingi zaidi
Tangu kusajiliwa MALAS mwaka 2024, tumeweza kuwafikia vijana kadhaa vyuoni na nje ya chuo ambao utalii ndiyo ilikuwa kitovu cha muunganiko huo. Mpaka Januari 2025 MALAS imepata wanachama wengi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM). Wanachama wengine ni kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, na Mtwara.
Bado safari inasonga mbele kwani tunatamani kuwa na watu ambao wanatazama uandishi wa vitabu na makala za utalii kama fursa ndani ya sekta ya utalii kwa sababu utalii na utamaduni vitaenezwa kupitia lugha ya maandishi. Tunakaribisha makundi yote ndani ya jamii kuungana nasi kwenye timu ili kwa pamoja tujivunie na kuutangaza utalii kati ya mataifa.